EAC Logo

 
 
Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt Hussein Mwinyi ikitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa siku ya kiswahili duniani Unguja, Zanzibar.

“Ongeza jitihada za kuimarisha lugha ya Kiswahili,” nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zashauriwa

Jumuiya ya Afrika Mashariki, Arusha, Tanzania, 7th July, 2022: Maelfu ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili toka Jumuiya ya Afrika Mashariki wamewaomba wakuu wa nchi za Jumuiya, kuongeza jitihada za kuiimarisha lugha ya Kiswahili na kubuni mbinu bora za kukuza na kuiendeleza lugha hii. 

Wito huo ulikaribishwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Zanzibar, Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi, aliyekuwa mgeni wa rasmi katika hafla ya  kuadhimisha Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, iliyofika kilele chake  leo, tarehe 7 Julai, 2022, Zanzibar. 

“Tuna wajibu wa kwanza sisi wenyewe Waswahili kuonesha mapenzi ya lugha yetu hii kwa kuizungumza kwa ufasaha na usahihi ili tuwe walimu wazuri kwa wale wanaojifunza.,” alisema Rais. 

Aidha, Mhe.Mwinyi ametoa wito kwa taasisi zinazosimamia maendeleo ya Kiswahili, kushirikiana katika masuala mbali mbali ya kuiendeleza lugha ya Kiswahili ikiwemo kutoa mafunzo na kufanya tafiti za Isimu na Fasihi ili kusaidia watunzi wa vitabu na machapisho yatakayosaidia kufunza Kiswahili. 

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshaanza kutoa ushirikiano wa aina mbali mbali kwa  Kamisheni ikiwa ni pamoja na kutoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika ya Mashariki hapa Zanzibar,” aliongeza Rais. 

 (K-L) Rais wa Zanzibar Mhe.Dkt Hussein Mwinyi, Mke wa Rais, Mama Mariam Mwinyi na baadhi ya wageni waalikwa wasikiliza maelezo ya mmoja baadhi ya waonyeshaji bidhaa kwenye viwanja vya Maadhimisho ya Kiswahili,Zanzibar.

Hafla ya maadhimisho ya lugha ya kiswahili duniani yaliyoanza jana kwa mara ya kwanza, imewaleta pamoja wawakilishi wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki, mabaraza ya Kiswahili, wahimizaji wa utumizi wa lugha ya Kiswahili kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki wakiwemo mawaziri, wajumbe, walimu, wanafunzi na wanahabari. 

Maadhimisho haya yamendaliwa na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (East Africa Kiswahili Commission) , taasisi iliyo chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community). 

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote akitoa salamu kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote , akimuwakilisha Katibu Mkuu Dkt. Peter Mathuki alisema kuwa moja ya mapendekezo ya Kongamano la Kiswahili lililofanyika jana, ni kuandaa mkutano maalumu wa Kiswahili wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  

“Lengo la kongamano hili litakuwa kuangalia namna ya kuboresha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki. Hii inajumuisha nchi wanachama kutenga bajeti ya tafiti na kujenga uwezo wa wataalamu wa lugha ya Kiswahili,“ Mhandisi Mlote alisema. 

Naibu Katibu Mkuu pia alisisitizia kuwa dhamira kuu ya Kamisheni ya Kiswahili ni kuhimiza na kuratibu maendeleo na matumizi ya Kiswahili kwa umoja wa kikanda na maendeleo endelevu ya jamii. 

“Kamisheni inajukumu kubwa la kuimarisha mawasiliano kwa kutumia Kiswahili kitaifa, kikanda na hata nje ya Jumuiya yetu.  Kamisheni pia ina wajibu wa kuzishauri nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa utangamano na maendeleo ya kikanda,“ aliongeza. 

Baadhi ya Washiriki wa maadhimisho ya Kiswahili Zanzibar wakifuatilia mkutano

Maadhimisho ya lugha ya Kiswahili yenye Kauli Mbiu: Kiswahili kwa Amani, Ustawi na Utangamano wa Kikanda yanatokana na uamuzi wa Kikao cha 41 cha Shirika la Umoja wa Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) uliofanyika tarehe 5 Novemba 2021. Uamuzi huo umeipa lugha ya Kiswahili kipaumbele kwa kuridhia maombi ya kuwa na Siku ya Kiswahili Duniani. Kutokana na uamuzi huo Siku ya Kiswahili Duniani itaadhimisha 7 Julai kila mwaka.  

Zanzibar ilipewa nafasi ya kwanza ya kuandaa maadhimisho ya Kiswahili,kwa kuzingatia kuwa Zanzibar ndio makao makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA), tahasisi iliyo chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  yenye makao yake makuu Zanzibar.   

 

For more information, please contact:

Simon Peter Owaka
Senior Public Relations Officer
Corporate Communications and Public Affairs Department
EAC Secretariat
Arusha, Tanzania
Tel: +255 768 552087
Email: sowaka [at] eachq.org

About the East African Community Secretariat:

The East African Community (EAC) is a regional intergovernmental organisation of six Partner States, comprising Burundi, Kenya, Rwanda, South Sudan, Tanzania and Uganda, with its headquarters in Arusha, Tanzania.

The EAC Secretariat is ISO 9001: 2015 Certified


East African Community
EAC Close
Afrika Mashariki Road
P.O. Box 1096
Arusha
United Republic of Tanzania

Tel: +255 (0)27 216 2100
Fax: +255 (0)27 216 2190
Email: eac@eachq.org