20th Anniversary Banner

 
 

Jumuiya ya Afrika Mashariki yaadhimisha Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani

Jumuiya ya Afrika Mashariki, Arusha, Tanzania, 8 Julai, 2025.; Mamia ya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili kutoka ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wameshiriki maadhimisho ya nne ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, jijini Kigali, Rwanda. 

Maadhimisho hayo ya siku mbili, yaliwaleta pamoja wahimizaji wa utumizi wa lugha ya Kiswahili kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki wakiwemo wabobezi wa kiswahili kutoka vyuo vikuu, wanafunzi na wanahabari kujadili pamoja umuhimu wa ukuaji na maendeleo ya lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki

Maadhimisho hayo ya nne lugha ya Kiswahili duniani yenye kauli mbiu: Kiswahili, Elimu Jumuishi na Maendeleo Endelevu pamoja na mengine matatu yaliyopita, yanatokana na uamuzi wa Kikao cha 41 cha Shirika la Umoja wa Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) uliofanyika tarehe 5 Novemba 2021 jijini Paris, Ufaransa. Kikao hicho kilitangaza Julai 7 kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani.

Kwa mujibu UNESCO Kiswahili kina wazungumzaji takribani milioni 230 duniani kote na ndio lugha ya Afrika iliyoenea zaidi katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Maadhimisho hayo ya nne yamendaliwa na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (East Africa Kiswahili Commission), taasisi iliyo chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community). 

pr 07082025 11

Akizungumza katika shamrashamra za maadhimisho hayo ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, Naibu waziri wa Elimu  kutoka Rwanda, Mh. Claudette Irene alisema Kiswahili ni zaidi ya lugha. Ni daraja linalowaunganisha watu zaidi ya milioni mia mbili katika bara la Afrika. Aliongeza kusema, Kiswahili kinadumisha ushirikiano wa kikanda, kinaimarisha mawasiliano, na kinakuza utambulisho wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa pamoja katika kuendeleza malengo ya pamoja ya amani, ustawi, na maendeleo ya wananchi.

Akiongelea jitihada mbalimbali za kukuza lugha ya Kiswahili nchini Rwanda, Mh. Irene aliongeza kusema Rwanda inatambua umuhimu wa Kiswahili katika kufanikisha elimu jumuishi na yenye usawa.

“Serikali yetu ilifanya auamuzi wa kihistoria mwaka 2017 kwa kufanya Kiswahili kama mojawapo ya lugha rasmi pamoja na Kinyarwanda, Kiingereza, na Kifaransa. Hatua hii haikuwa tu ya ishara, bali ilikuwa ya makusudi na yakimkakati yenye nia ya kujenga mshikamano na undugu wa Kiafrika,” aliongeza Mh. Irene

Naibu Waziri aliwathibitishia washiriki kwamba Rwanda itaendelea kujitolea kukiendeleza Kiswahili katika elimu, biashara, diplomasia na kitamaduni. 

“Sote tuendelee kukipigania Kiswahili, sio tu kama lugha, lakini kama ishara ya uthabiti na umoja wa kiafrika.”

pr 07082025 11

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mheshimiwa Andrea Aguer Ariik Malueth alisema, “Kiswahili ni zaidi ya lugha, ni taswira ya jinsi tulivyo, huonyesha hisia zetu, huhifadhi tamaduni zetu na kujumuisha utambulisho wetu wa pamoja. Ni lugha ambayo tunaishi nayo, na kujenga jamii zetu.”

“Tunapoadhimisha siku hii muhimu, tuthibitishe dhamira yetu ya kukuza Kiswahili sio tu kama nyenzo ya mawasiliano, bali kama nguzo muhimu ya umoja, amani na maendeleo katika eneo letu,’’ aliongeza Naibu Katibu Mkuu.

Mh. Malueth aliwakumbusha washiriki wa maadhimisho hayo kwamba Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulipitisha Kiswahili kama mojawapo ya lugha rasmi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Vilevile Mkutano wa 24 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliidhinisha marekebisho ya Ibara ya 137 ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuongeza lugha ya Kiswahili na Kifaransa kama lugha rasmi za Jumuiya baada ya Kingereza.

Naibu Katibu Mkuu huyo aliongeza kusema kuwa katika nchi nyingi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kiswahili kimekubaliwa kuwa lugha rasmi au ya taifa na kinafundishwa shuleni katika ngazi mbalimbali.

“Tunaziomba nchi wanachama kuongeza juhudi zaidi katika kufundisha Kiswahili katika mifumo wa shule, kwani hii itahakikisha kwamba vijana wetu wanakua na fikra na mitazamo ifaayo kwa Kiswahili,” alisema Mhe. Malueth.

pr 07082025 11

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Daktari Caroline Asiimwe, alisema Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki imejitolea kuhakikisha kwamba inafanikisha juhudi za kukiendeleza Kiswahili, siyo tu katika ukanda Jumuiya ya Afrika Mashariki, bali duniani kote.

Aliongeza kusema kuanzishwa kwa Kamisheni ya Kiswahili ni ushahidi kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki inatambua umuhimu wa Kiswahili katika kufanikisha utangamano wa kikanda na kuwezesha maendeleo endelevu.

“Kama taasisi iliyopewa jukumu la kuendeleza lugha ya Kiswahili ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, tutajitahidi kutoa ushauri kwa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na nchi wanachama kwa kutumia ushahidi wa kisayansi kupitia utafiti ili kuimarisha sera, mipango na maendeleo ya lugha ya Kiswahili,” alisema Dkt. Asiimwe.

pr 07082025 11

Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Masharili ulipitisha tamko la Julai 7 kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani na kuagiza iadhimishwe kila mwaka kwa mzunguko kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Maadhimisho ya kwanza ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani yalifanyika Zanzibar, Tanzania kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022. Maadhimisho ya pili yalifanyika Kampala, Uganda kuanzia tarehe 5 – 7 Julai, 2023, na Maadhimisho ya tatu yalifanyika Mombasa, Kenya kuanzia tarehe 5 – 7 Julai, 2024.

 

For more information please contact:

Florian Mutabazi
Media Coordinator
Corporate Communications and Public Affairs Department
EAC Secretariat
Arusha, Tanzania
Tel: +255 785288428
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

About the East African Community Secretariat:

The East African Community (EAC) is a regional intergovernmental organisation of eight (8) Partner States, comprising the Republic of Burundi, the Democratic Republic of Congo, the Republic of Kenya, the Republic of Rwanda, the Federal Republic of Somalia, the Republic of South Sudan, the Republic of Uganda and the United Republic of Tanzania, with its headquarters in Arusha, Tanzania. The Federal Republic of Somalia was admitted into the EAC bloc by the Summit of EAC Heads of State on 24th November, 2023 and became a full member on 4th March, 2024.

Tags: East African Kiswahili Commission (EAKC), #SikuYaKiswahiliDuniani


East African Community
EAC Close
Afrika Mashariki Road
P.O. Box 1096
Arusha
United Republic of Tanzania

Tel: +255 (0)27 216 2100
Fax: +255 (0)27 216 2190
Email: eac@eachq.org