EAC Logo

 
 

Maswali ya Mara kwa Mara na Majibu kuhusu UVIKO-19

Imechapishwa Aprili 3, 2020

Mnamo Januari 2020 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa ugonjwa mpya wa virusi vya korona katika Mkoa wa Hubei, Uchina, kuwa suala la Hali ya Hatari ya Afya ya Umma Kimataifa kwa sababu ya uwezekano mkubwa wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona vya mwaka 2019 (UVIKO-19) kuenea duniani kote. Kufikia Aprili 2 2020, wagonjwa zaidi ya 896, 450 wameambukizwa katika nchi zaidi ya 200, zaidi ya watu 45, 526 wamekufa kutokana na ugonjwa huo, lakini wengine 135,000 pia wametibiwa na kupona tangu kuzuka kwa ugonjwa huo. Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki matukio ya ugonjwa huu wameripotiwa nchini Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda na Tanzania. Watu wengi walioambukizwa huonyesha dalili zisizo kali na kiwango cha takribani 4% cha vifo ulimwenguni ni cha chini kikilinganishwa na magonjwa mengine ya kuambukiza yanayotokea ukanda huu kama vile VVU/UKIMWI, surua au Ebola. Janga hili  halijaathiri tu sekta ya afya, bali limeathiri uchumi kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na biashara na utalii, ambazo ndio nguzo kuu za maisha katika ukanda huu.

Ili kufanikiwa katika kukabiliana na janga hili, makundi yote katika jamii yetu ikiwa ni pamoja na waajiri na wafanyabiashara – ni lazima yahusike na kushirikiana. Kirusi ambacho husababisha Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) ni cha aina mpya ambacho hakikuwa kimewahi kutokea kwa binadamu hadi ugonjwa huo ulipozuka mwaka wa 2019.

Virusi vya Korona (ViKo) ni kundi kubwa la virusi ambavyo kwa kawaida hupatikana kwa wanyama na husababisha maradhi hatari yanyohusiana na upumuaji kama vile Dalili za Upumuaji za Middle East (Middle East Respiratory Syndrome (MERS-CoV) na Dalili Kali na Hatari za Upumuaji (Severe Acute Respiratory Syndrome (SARS- CoV).

Virusi vya korona huambukizwa baina ya wanyama na watu. Uchunguzi wa kina ulibaini kuwa virusi vikali na hatari vya SARS-CoV viliambukizwa binadamu kutoka paka aina ya ngawa navyo virusi vya upumuaji vya MERS-CoV viliambukizwa binadamu kutoka ngamia wenye nundu moja. Kuna virusi vya korona vingine vinavyojulikana kuwa vinapatikana miongoni mwa wanyama bila kusababisha ugonjwa kwa binadamu.

Mlipuko wa UVIKO-19 umeathiri vibaya nchi nyingi duniani na umesababisha hasara kubwa katiak sekta mbalimbali za kiuchumi.

Katika sehemu ifuatayo tunatoa majibu ya maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu UVIKO-19:

 

+  Virusi vya Korona ni nini?

Virusi vya korona ni kundi kubwa la virusi ambayvo kwa kawaida hupatikana miongoni mwa wanyama na vinaweza kusababisha ugonjwa kwa wanyama na binadamu. Kwa binadamu, virusi vya korona husababisha magonjwa ya kupumua kama vile homa ya kawaida isiyo na dalili kali na Dalili za Upumuaji za Middle East (Middle East Respiratory Syndrome (MERS) na Dalili Kali na Hatari za Upumuaji (Severe Acute Respiratory Syndrome (SARS). Virusi vilivyopatikana hivi karibuni husababisha Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.
 

+  Nini maana ya UVIKO-19?

UVIKO-19 ni kifupisho cha Ugonjwa wa Virusi vya Korona. Katika Kiingereza, UVIKO ni COVID (Corona Virus Disease). Katika kifupisho UVIKO-19, 'U' kinawakilisha 'Ugonjwa,' 'VI' 'Virusi,' na 'KO' ni Korona. Jina ‘COVID’ linafuata taratibu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za kutaja magonjwa mapya ya kuambukiza kwa binadamu.
 

+  UVIKO-19 ni nini?

Ugonjwa wa Virusi vya Korona unafanana na homa ya mafua inayoambukizwa kwa kasi mno.
 

+  Nini dalili za UVIKO-19?

Dalili za kawaida za UVIKO-19 ni homa, uchovu, na kikohozi kikavu. Baadhi ya wagonjwa wanaweza kuwa na maumivu na uchungu, kubanwa pua, kutokwa kamasi, vidonda kooni au kuhara. Mara nyingi dalili hizi huwa si kali na huanza polepole. Watu wengine huambukizwa lakini hawaonyeshi dalili zozote na huwa hawajisikii vibaya. Watu wengi (takribani asilimia 80) hupona kutokana na ugonjwa huu bila kuhitaji matibabu maalum. Ni kama mtu mmoja kati ya watu sita wanaopata UVIKO-19 ndiye hudhoofika na kutatizika kupumua.
 

+  Ni nani aliye katika hatari kubwa zaidi ya kupata UVIKO-19?

Mtu yeyote anayekumbana na virusi vinavyosababisha UWIKO-19 yuko hatarini. Hata hivyo, watu wa umri mkubwa, na wale walio na hali nyingine za kiafya kama vile shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na ugonjwa wa kisukari au wale ambao kinga ya mwili imedhoofika, kama vile watu walio na VVU/UKIMWI au saratani, wako katika hatari zaidi na wana uwezekano mkubwa wa kupata dalili kali.
 

+  Ninahitaji kuhofia watoto wangu?

Visa vya watoto kuambukizwa vimeripotiwa. Hata hivyo, watoto na hata vijana hawaonekani kuathiriwa sana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona kama ilivyo kwa wazee.
 

+  UVIKO-19 husambaa vipi?

Ugonjwa huu unaweza kusambaa kutoka mtu mmoja kwenda mtu mwingine kupitia vitonetone wakati mtu aliyeambukizwa anapopiga chafya, anapokohoa au anapopumua. Wakati mwingine watu huambukizwa UVIKO-19 wanapogusa vitu au sehemu yenye virusi na kujigusa machoni, puani au mdomoni.
 

+  Ninaweza kujikinga vipi ili nisiambukizwe?

Njia bora ya kuzuia kuambukizwa ni kuepukana na kukumbana na virusi. Hili linawezekana kwa kuzingatia hali ya juu ya usafi, kuepuka kugusana na watu walioambukizwa na kujitenga na watu wengine kwa umbali wa futi 6, kwa sababu virusi hivyo husambaa mara nyingi kutoka mtu mmoja hadi kwa mwingine na baina ya watu waliokaribiana. Hili ni muhimu sana haswa kwa watu ambao wako katika hatari kubwa ya kuwa wagonjwa.
 

+  Ni hatua gani za usafi zilizo muafaka?

  • Safisha mikono yako mara kwa mara kwa kuiosha kwa sabuni na maji kwa angalau sekunde 20, haswa baada ya kuwa mahali pa umma, au baada ya kusafisha pua, kukohoa, au kupiga chafya.
    • Unaweza pia kutumia kitakasa mikono ambacho kina angalau asilimia 60 ya kileo. Sugua mikono yako mpaka ikauka.
    • Usijiguse machoni, puani na mdomoni kwa mikono isiyooshwa.

+  Ninahitaji kuvaa barakoa ili nijikinge na virusi hivi?

Huhitaji kuvaa barakoa kama wewe si mgonjwa au unamhudumia mgonjwa (ambaye hawezi kuvaa barakoa). Barakoa ziachiwe wale wanaozihitaji.
 

+  Ninaweza kufanya nini kuwakinga wengine iwapo mimi ni mgonjwa au nimepatikana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona?

kiwa unaugua, usitoke nyumbani, isipokuwa pale unapohitaji huduma ya matibabu, hata kama haijathibitishwa kwamba umeambukizwa Virusi vya Korona au una homa ya kawaida. Pia:
  • Funika mdomo na pua kwa kitambaa wakati unapokohoa au kupiga chafya au fanya hivyo ndani ya kiwiko chako na ukioshe baadaye.

  • Tupa kifaa kilichotumika kwenye takataka.

  • Bila kuchelewa nawa mikono yako kwa sabuni na maji kwa angalau sekunde 20 au safisha mikono kwa kutumia kitakasa mikono chenye angalau silimia 60 ya kileo.

  • Vaa barakoa unapokuwa karibu na watu wengine (k.m. mnapotumia chumba kimoja au gari na kabla ya kuingia kwenye kituo cha afya.

  • Kwanza safisha halafu takasa kila siku sehemu zinazoguswa mara kwa mara, kama vile meza, vitasa vya milango, swichi za umeme, mipini, dawati, simu, kibodi, vyoo, bomba na sinki za maji.

+  Mtu aliyeachiliwa kutoka karantini ya UVIKO-19 anaweza kusambaza ugonjwa huo?

Mtu ambaye ameachiliwa kutoka karantini ya UVIKO-19 hana hatari ya kueneza virusi kwa sababu hakuonyesha dalili wakati wa kipindi alichokuwa amezuiliwa.

Maana ya karatinti ni kumtenga mtu (au kikundi cha watu) na watu wengine aliyekumbana na ugonjwa wa kuambukizwa lakini ambaye hajaonyesha dalili ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Karantini kwa kawaida hutegemea urefu wa kipindi cha ugonjwa wa kuambukizwa, ambao ni muda wa watu kuonyesha dalili za ugonjwa. Kwa UVIKO-19 kipindi hiki ni siku 14 kutoka tarehe ya mwisho kukumbana na ugonjwa huu, kwa kuwa siku 14 ndicho kipindi kirefu zaidi cha kupevuka kinachoonekana kwa virusi vingine vya aina hii ya korona.

+  Ni kwa namna gani ninaweza kuchangia kuzuia unyanyapaa wa watu wenye virusi vya UVIKO-19?

Hofu na wasiwasi vinaweza kusababisha unyanyapaa-kijamii, kwa mfano, kwa watu waliokuwa karantini ya UVIKO-19. Unyanyapaa unatokana na kutokuwa na habari kamili kuhusu UVIKO-19 na jinsi unavyoenea au kutokana na udaku na uzushi. Unaweza kuzuia unyanyapaa na kusaidia wengine kwa kutoa msaada wa kijamii.

Unaweza kupigana na unyanyapaa na kuwasaidia, na siyo kuwadhuru, wengine katika jamii. Unaweza kupinga unyanyapaa kwa kujifunza na kuwafunza wengine ukweli, kwa mfano kwamba virusi havilengi makundi fulani ya jamii.

Toa taarifa mpya kuhusu UVIKO-19 kwa wenzako lakini epukana na kueneza uongo.
 

+  Kuna tiba ya UVIKO-19?

Hakuna tiba maalum ya UVIKO-19. Usiwaamini watu wanaojaribu kukuuzia dawa na kuahidi kwamba watauponya ugonjwa huo. Magonjwa ya virusi yanaweza kuzuiwa na chanjo ikipatikana, lakini hayawezi kuponywa kwa kutumia viuavijasumu. Hata hivyo, matibabu au tiba inaweza kusaidia kupunguza dalili zinazoambatana na virusi, kama vile homa au kikohozi.
 

+  Kuna chanjo dhidi ya UVIKO-19?

Kufikia sasa, hakuna chanjo dhidi ya UVIKO-19. Wagonjwa watapata msaada na uangalizi kutoka kwa wahudumu wa afya hadi watakapopona.
 

+  Ni lazima niogope UVIKO-19?

Kila ugonjwa wa virusi ni hatari na UVIKO-19 unaambukizwa kwa wepesi sana. Ugonjwa huu unaweza kuenea kwa haraka mno na kuambukiza watu wengi katika kipindi kifupi. Hata hivyo, dalili za UVIKO-19 mara nyingi huwa si za kutisha. Wagonjwa wengi huwa hawaonani na daktari. Kiwango cha asilimia 4 ya vifo vya UVIKO-19 kinachotokea ni cha chini kikilinganishwa na magonjwa mengine ambayo yanatokea katika ukanda huu. Kwa Mfano: Kiwango cha vifo vya ugonjwa wa surua au virusi vya Ebola kinaweza kuwa zaidi ya asilimia 60 na hadi asilimia 100 ya watu wanaoambukizwa kichaa cha mbwa watakufa.

Mfano mwingine: Nchi ya Uchina, yenye watu zaidi ya bilioni 1.4, ni watu 80,000 tu ambao wamethibitishwa kuwa na UVIKO-19.

+  Ninaweza kufanya nini kuhakikisha maeneo ya kazi ni salama kwangu na kwa wenzangu?

Ikiwa UVIKO-19 utafika kazini kwako, unaweza kusimamisha au kuzuia kuenea kwake kwa kupunguza siku za kufanya kazi:
  • Hakikisha umedumisha usafi kila sehemu kazini kwako (k.m. madawati na meza) na vitu (k.m simu, kibodi). Vifute na vitakasa mara kwa mara.

  • Himiza wafanyikazi na wageni kuosha mikono kwa makini mara kwa mara.

  • Hakikisha maeneo ya kazi yana nafasi za kutosha kuruhusu hewa safi kuzunguka (usafi mzuri wa kupumua).

+  Ni salama kutumia usafiri wa umma (Daladala au Matatu) kipindi hiki cha UVIKO-19?

Abiria katika Matatu au Daladala huwa wamesongamana na hakuna njia ya kutenga nafasi baina ya abiria mmoja na yule anayekohoa na kupiga chafya na kuzuia kusambaa kwa vitonetotone kutoka pua yake na mdomo wake. Kwa hivyo, utumiaji wa usafiri wa umma una hatari kubwa ya maambukizi ya UVIKO-19 na magonjwa mengine ya kuambukiza. Ikiwezekana, usafiri mbadala utumiwe kana njia ya kuzuia maambukizi wakati huu wa UVIKO-19.
 

+  Ninaweza kuhudhuria ibada?

Huu ni uamuzi wa kibinafsi. Kwa hakika, ibada inaweza kusaidia kuenea maambukizi kwa kuwa watu wengi hukusanyika na kukaa na kusimama karibu-karibu.Ukifikiri kuwa kuhudhuria ibada ni bora kuliko kujikinga dhidi ya UVIKO-19, basi huo utakuwa uamuzi wako binafsi. Ukiamua kuhudhuria ibada, jitenge na washiriki wenzako kadri iwezekanavyo na epuka kusalimiana. Unaweza pia kumhusisha kiongozi wako wa dini katika kulishughulikia janga hili. Ikiwa tayari una UVIKO-19, KAMWE usiende kwenye ibada, kwa kuwa utahatarisha usalama wa wenzako.
 

+  Waafrika wana kinga dhidi ya UVIKO-19?

Habari zisizo za kweli vimeanza kuibuka kuhusu UVIKO-19. Mojapo ni kwamba Waafrika wana kinga dhidi ya UVIKO-19. Usiamini habari kama hizo. Ugonjwa huu haumbagui mtu yeyote. Tayari zaidi ya nchi 35 za Afrika zimeripoti matukio ya visa vya UVIKO-19, uthibitisho kwamba hakuna usalama bila tahadhari na kujikinga.
 

+  Je, kula nyama ya mwituni kuna hatari ya maambukizi ya UVIKO-19?

Nyama ya mwituni inadhaniwa kuwa chanzo cha janga la sasa la virusi vya korona. Virusi vya korona na bakteria nyingine hujitokeza kwa kawaida katika wanyama. Kwa hivyo, mchakato wa kuandaa nyama ya kula unahitaji kufuata kanuni za maandalizi safi na salama ya chakula. Nyama inapaswa kukaguliwa na wataalam wanaohusika na watumiaji wanashauriwa kuiandaa vizuri, kwa kupika au kuikaanga ili iive na isiwe mbichi.
 

+  Wagonjwa waliopona kutokana na UVIKO-19 wana kinga dhidi ya virusi hivyo?

Ni mapema mno kutoa jubu la uhakika. Hata hivyo, kuna ushahidi wa kisayansi unaonyesha kuwa mtu aliyeambukizwa UVIKO-19 na kupona hujenga aina fulani ya kinga dhidi ya mbegu ya kirusi iliyosababisha maambukizi. Wanasayansi nchini Uchina kwa makusudi waliambukiza nyani aina ya ngedere UVIKO-19 na pia wakawaambukiz ngedere walionusurika kiwango kikubwa cha virusi. Hakuna ngedere aliyeambukizwa mara ya pili aliyekuwa mgonjwa. Mkabiliano wa kujikinga na maradhi wa ngedere unafanana kwa kiasi fulani na ule wa binadamu. Hivyo, wataalamu kwa makini wanafasiri matokeo ya jaribio hilo kumaanisha kuwa binadamu aliyepona UVIKO-19 akiambukizwa tena hawezi kuathirika sana..
 

+  Bidhaa kutoka Uchina ni salama?

Majaribio ya kisayansi yalionyesha kuwa virusi vinavyosababisha UVIKO-19 vinaweza kuishi kwa nguo au sehemu ya juu ya kitu kwa saa kadhaa, kutegema hali nyingine kama vile kiwango cha joto, unyevunyevu na kadhalika. Iwapo bidhaa kutoka Uchina vitakuwa vimechafuliwa na virusi huwa vinasafiri masafa marefu kabla kufika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hivyo, itakuwa vigumu kwa virusi hivyo kuwa bado hai. Hata hivyo, ikiwa maana ya ‘bidhaa’ ni pamoja na wanyama hai walio na virusi, bila shaka maambukizi yanaweza kutokea. Hivyo, Uchina imeweka marufuku ya biashara ya kigeni ya wanyama wa mwituni.
 

+  Ninaweza kupata UVIKO-19 kwa nguo kuukuu kutoka ng’ambo?

Virusi vinavyosababisha UVIKO-19 vinaweza kuishi kwa nguo au sehemu ya juu ya kitu kwa saa kadhaa, kutegema hali nyingine kama vile kiwango cha joto au unyevunyevu. Hata hivyo, iwapo nguo kuukuu zilitoka ng’ambo, zilisafiri masafa marefu na zitakuwa zilisafishwa na kuwekwa dawa ya kuua viini vya maradhi kabla ya kuuzwa kama inavyopendekezwa na viwango vya biashara ya kimataifa. Kwa hali hii, ni vigumu kwa virusi kupatikana katika nguo kuukuu.
Ikiwa bado una shaka na unataka uhakika na kuwa salama kabisa, osha nguo hizo kwa kutumia sabuni ya unga kwenye maji moto ya digrii 60 au zaidi. Hii itaviua virusi.
 

https://www.who.int/news-room/q-a-detail/q-a-coronaviruses

https://www.cdc.gov/coronavirus/2019-ncov/faq.html

Tags: COVID-19


East African Community
EAC Close
Afrika Mashariki Road
P.O. Box 1096
Arusha
United Republic of Tanzania

Tel: +255 (0)27 216 2100
Fax: +255 (0)27 216 2190
Email: eac@eachq.org